Wednesday, August 26, 2009

MAFANIKIO KATIKA NDOA

Badala ya watu kuangalia dosari katika ndoa za wengine, kwanini wasitazame mafanikio katika ndoa nyingine. Kuna mengi ya kujifunza badala ya mengi ya kukosoa.

Wengi hupenda kutazama ndoa zilizofeli, wakijaribu kudadisi kwa nini ndoa hizo zimeshindwa na lengo lao sio kutoa msaada bali lengo ni kufurahisha genge. Lakini jambo la ajabu watu hao huzifumbia macho ndoa zilizofanikiwa.

Katika makala haya, tutajaribu kutoa ushauri uliotokana na utafiti ili watu watazame zaidi ndoa zilizofaulu na kuyatambua mambo ya msingi yanayojenga na kudumisha maisha mema ya ndoa.

Sisi, kwa kuyatazama mambo haya ya maana, tumebaini virutubisho muhimu vya maisha ya ndoa ambavyo vinaweza kumpatia kila mwanandoa furaha inayotafutwa mno katika maisha hayo. Hapa kuna mambo manane:

1. Dhati ya moyo na Upendo wa dhati (Eternal Commitment and caring)

Ndoa zinazojengwa kwa msingi wa dhati ya moyo (commitment) huwa katika mazingira ya usalama ambayo huwapa wanandoa wasaa wa kujistawisha na kufanikiwa kwa kiwango kinachozidi uwezo walionao.

Nao upendo wa dhati maana yake ni hisia za kila mmoja kumjali mwingine pengine kuliko hata anavyoijali nafsi yake. Hisia hizi hufuta ubinafsi moyoni na kumfanya kila mmoja aangalie shida na mahitaji ya mwingine kuliko anavyoangalia shida na mahitaji yake binafsi.

Mume na mke waishi katika mawimbi ya hisia kila mmoja ajaribu kumzidi mwingine hisia za kumjali mwenza, hapa maisha ya ndoa yatakuwa ya furaha kwelikweli na ndoa hiyo, InshaAllah, itadumu na kama itavunjika basi ni kwa sababu za msingi za kibinadamu.

Wanandoa katika ndoa za namna hii, mara nyingi, hutenganishwa na kifo. Ndoa hizi huwa na mvuto kwa wengine na huandaa mazingira bora ya kizazi kipya ambacho, kwa vyovyote, kitakuwa na nguvu kubwa ya maadili itakayowavutia wanajamii kwa ujumla.

Lakini ubinafsi wa kila mmoja kujitazama yeye tu bila kumjali mwenza huondosha imani ya kila mmoja kwa mwingine na hujenga mtindo mbaya wa ‘chukua chako, nichukue changu’

Kila mmoja hutanguliza mbele maslahi yake na humtimizia mwingine haja zake pale anapoona kuna maslahi kwake. Wanandoa hufikia mahala pa kuwekeana masharti, bila mmoja kufanya kitu fulani basi mwingine naye hawezi kufanya kitu fulani. Hata unyumba hufanyika kwa masharti.

Kwa hiyo basi, dhati ya moyo na upendo wa dhati ndizo sifa za msingi za ndoa yenye mafanikio. Msukumo ulio nyuma ya sifa hizi ni uadilifu. Uadilifu wa wanandoa ndio unaoimarisha ndoa na kuipa nguvu ya kudumu.

Ni jambo la kuzingatia mno kuwa ndoa ni mkataba lakini mkataba huu hauna uhai wa kujitegemea, uhai wa mkataba huu si wa cheti cha ndoa wala si wa sherehe za harusi bali umo katika nyoyo za wale wanaoufunga.

Ndoa, katika Uislamu, ni mkataba baina ya wanandoa. Huu ni mkataba ambapo kila upande lazima uwajibike na majukumu yake. Tija ya mkataba huu wa hiyari hutegemea athari za kupendana na kuhurumiana kwa wanandoa.

Wanandoa jengeni maisha yenu ya ndoa sio kwa mapenzi yanayoambatana na masharti bali kwa utamaduni wa hisani. Toa kwa ajili ya Allah kwanza halafu toa kumpa mwenza bila kutarajia kurejeshewa malipo yoyote kutoka kwake.

Kila mwanandoa mwenye moyo wa dhati ashirikiane na mwenza kutekeleza majukumu ya msingi na kufanya kazi za kila siku. Kila mmoja ajitahidi kuonesha ushirikiano wa asilimia 100.

Kigezo chetu bora ni maisha ndoa ya Mtume sallallahu alayhi wa sallam na Bi Khadija. Bi Khadija alimsaidia Mtume kwa mali yake na akamsaidia nyumbani.

2. Mawasiliano bora (Effective Communication Skills)

Mawasiliano ni muhimu zaidi kuliko maelewano. Wanandoa wanaweza kutofautiana mara nyingi lakini bado wakadumisha ndoa yao iwapo watawasilishiana hisia na fikra zao kwa njia bora.

Miaka ishirini na mitano ya utafiti inatubainishia kuwa mafanikio katika ndoa hayahusiani sana na aina ya tofauti baina ya wanandoa. “Ukitaka kuwa na ndoa yenye furaha, basi ni vema ujuwe zaidi njia ya kuyadhibiti mambo yanayoleta tofauti hizo kuliko hata kuzijua tofauti zenyewe”, hivi ndivyo wasemavyo Madaktari hawa, Dkt.Markman, Stanley na Blumbarg katika kitabu chao “Fighting for Your Marriage”

Kuweka wazi njia za mawasiliano baina ya wanandoa ili kubadilishana hisia zao nzuri na mbaya ni jambo muhimu mno. Wasilisha mawazo yako vizuri iwe kuhusu jambo jema au tatizo, eleza kwa lugha nzuri yale unayoyakubali na tumia lugha nzuri zaidi na ya hekima kueleza yale unayoyakataa.

Pale inapojitokeza hali ya kutoelewana, fanyeni mazungumzo ya wazi kudhibiti hali ya mambo mkitumia stratejia ya kulishinda tatizo, ‘win-win strategy’

Katika programu yake Mashuhuri ya Mafunzo iitwayo, “seven Habits of Highly effective People”, “Tabia Saba za Watu wenye busara ya hali ya juu”, Bw. Steven Covoy anasema, “Win-Win”is a paradigm of human interaction that comes from integrity, maturity and abandance mentality.”Busara ni mabadiliko katika maisha ya mwanadamu ambayo huja kutokana na uadilifu, upevu na wingi fikra.”

Kwa mawasiliano bora unaweza kukifikia kiwango cha unyumba (intimacy) unachokitaka. Mahusiano na mashirikiano bora katika nyumba huwezekana iwapo mume na mke watakuwa wazi kwa kila mmoja wao. Pale kila mmoja wao anapomuamini mwenziwe na anapoaminiwa na mwenza, wote wawili huweza kuwasilishiana fikra na hisia zao bila kitete (reservation).

3. Amani ya Hisia (Emotional Safety)
“Kuonesha amani ya hisia ni jambo la msingi katika kujenga mahusiano ya dhati ya ndoa yenye mapenzi ambayo wewe unaitaka.” Hivi ndivyo wanavyosema Madaktari, Markman, Stanley na Blumberg.

Hapa wana maana ya mume na mke kuishi kwa heshima, huruma na mapenzi. Pale wanandoa wanapokumbana na tatizo au hali fulani ngumu iwe ya nje au ya ndani, wafanye kila jitihada kujizuia na ghadhabu na kinyongo.

Katika nyakati hizi ngumu, wajitahidi kufichiana siri na kusitiriana. MwenyeziMungu anasema wao (wanawake) ni nguo kwenu na nyinyi ni nguo kwao”. (2:187).

Wanandoa Waislamu wasaidiane hasa hasa katika nyakati ngumu. Pale watu wengine wanapomtelekeza, basi mtu hujirudisha kwa mwandani wake ili apate kumfariji na kumpa nguvu ya kukabiliana na hali ngumu aliyonayo na kuendelea na safari yao ya maisha.

Mama wa Waumini yaani wakeze Mtume sallallahu alayhi wa sallam walikuwa karibu na Mtume katika matatizo na mapambano aliyokabiliana nayo.



4. Kudumu na matarajio halisi (Developing Realistic Expectation)

Achana na njozi (ideal image) ya kuwa na mume ambaye hawezi kupatikana katika dunia hii. Ndugu yetu mmoja katika Uislamu alielezea uzoefu na uchunghuzi wake katika miaka miwili ya ndoa yake akisema; “The fastest path to destroying one’s marriage is false hopes and ideals that we make for ourselves. For instance, we may think that another couple’s relationship is our inspiration and a model to copy. This may bring positive results in some instances and can lead to crisis in others”

Yaani “njia ya haraka zaidi ya kuvunja ndoa ya mtu ni imani na mawazo potofu tunayoyajenga sisi wenyewe (wanawake). Mathalani, tunaweza kudhani kuwa ndoa ya watu wengine ndiyo ya kutuongoza na ndio kigezo cha kuiga.. Hii yaweza kuleta tija katika ndoa fulani na kusababisha matatizo katika ndoa nyingine.”

5. Kuyaangazia mambo mema (Shining a Light on What is Right)

Tabia njema kwa mwenza ni moja ya zawadi ambazo mume na mke wanaweza kuiletea ndoa yao. Kwa kuridhiana, mume na mke humfanya kila mmoja wao kuwa mpenzi mkubwa wa mwingine.

“Hapa kuna msemo mmoja unaowahusu waume na wake, “kama unataka kumbadili umpendae, basi mpende. Kama mapenzi yako ni ya kweli, basi mumeo au mkeo atayahisi na yeye atashawishika moyoni kupenda, kujali na kuwa msaidizi.

6. Kuhisi na kuzingatia hisia na mahitaji ya mwenza (Sensitivity and Consideration to the spouse’s feelings and needs)

Igeuze kanuni hii, “Mtendee mwandani wako kama wewe unavyotaka kutendewa.” Badala yake fuata kanuni ambayo ni bora zaidi, “mtendee mwandani kama anavyotaka kutendewa.”

Jambo hili ni rahisi kulisema lakini gumu kulitenda. Ni jambo linalohitaji ufahamu sahihi na maridhiano ya kweli ya wanandoa. Jaribu kung’amua mambo yanayomfurahisha mwenza kwa kuyasoma maongezi yake mwenyewe.

Tia tone la maji katika ndoo ya mwandani wako ili kutia nyongeza katika benki ya hisia ya mwenza. Katika kitabu chao “How Full Is Your Bucket? Positive Strategies for Work and Life, Tom Rath na Donald Clifton waliutazama utafiti wa miaka hamsini wa Gallup pamoja na mamilioni ya mahojiano kuweza kujenga hoja kuwa uhusiano huu ‘wa nipe-nikupe’ give-and-take hujenga ndoa imara, huzidisha furaha na tija kwa mfanyakazi na hujenga ulimwengu wenye furaha zaidi.

Nadharia yao inasema hivi: “kila mmoja wetu ana ndoo yake iliyofichikana ambayo huwa tupu au hujaa katika maisha ya kila siku, hii hutegemea watu wengine wanavyotusemesha au kutufanyia jambo.

Ndoo yetu inapokuwa imejaa, tunakuwa na furaha, na ndoo yetu inapokuwa tupu, tunasononeka. Kila mmoja wetu pia ana kata lisiloonekana. Tunapotumia kata hiyo kujaza ndoo za wengine-kwa kusema au kufanya mambo yanayowapunguzia hisia njema- basi tunajipunguzia hisia hata sisi wenyewe.”

Wanandoa wanaofaulu kufahamu kila mmoja wao anahitaji nini ndio wenye uwezekano zaidi wa kuijiongezea kiwango cha hisia katika benki ya hisia. Katika mchakato huu tunatakiwa kujifahamu kabla ya kufahamika, kujielewa kabla ya kueleweka, kujitambua kabla ya kutambuliwa.

Ili kuweza kufanya hilo, jaribu kusikiliza kwa hisia. Epukeni kukaripiana, kupelelezana, kudhaniana na kukisiana.

7. Urafiki (Companionship)

Urafiki muhimu na wa kudumu muda mrefu ni ule wa wanandoa. Takribani yale yote yanayohusiana na uhusiano wa urafiki yamo katika uhusiano wa ndoa isipokuwa zipo tofauti.

MwenyeziMungu kawapangia mume na mke kuwa marafiki wa ndani. Mume na mke wanapokuwa marafiki, huweza kusaidiana kuikabili changamoto ya Uislamu ya kuishi kwa kufuata misingi na maadili yake ili kupata furaha katika dunia hii na Akhera.

MwenyeziMungu Anasema, “Na wanaoamini wanaume na wanaoamini wanawake ni marafiki wao kwa wao. Huyaamrisha yaliyo mema na kukataza yaliyo mabaya, na husimamisha Sala na hutoa Zaka na humtii MwenyeziMungu na Mtume Wake. Hao ndio ambao MwenyeziMungu atawarehemu. Hakika MwenyeziMungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima. (9:71).

Ili kufaulu kufikia lengo hili tukufu, tuache matamanio ya nafsi zetu na majivuno, na badala yake tuitazame dini yetu bila kujali nani anayeizungumzia, mwanaume au mwanamke, mzee au kijana mwanazuoni au mtu wa kawaida.

Tuipime hoja yake na kuitafutia uthibitisho wa Qur’an na Hadith Sahihi. Aidha inahitaji tujiepushe na athari za mazoea, maslahi binafsi na ubinafsi.

8. Kupanga ratiba (Making a schedule)

Kupanga ratiba kunatoa nafasi ya kuendesha maisha yenu kwa mpangilio bora. Hii hasa huwa muhimu zaidi iwapo mume na mke wanasoma au kufanya kazi.

Katika hali hii ratiba husaidia kutenga muda kwa kila mmoja katika siku za kazi na masomo. Ratiba inaweza kujumuisha mambo haya.

-Kusali pamoja angalau kipindi kimoja cha Sala
-Kuhudhuria pamoja darasa-duara mara moja kwa wiki.
-Kutenga siku moja ambapo kusiwe na kazi wala masomo, na badala yake kushughulika na yale yanayompendeza kila mmoja.
-Kutenga siku moja ambapo mume na mke kwa pamoja wafanye kazi ya usafi wa nyumba.
-Kutenga siku na muda wa kutembelea ndugu, jamaa, wagonjwa.
-Kutenga muda wa kujadili bajeti na kutatua matatizo.

Kwa kujipangia ratiba hii, wanandoa watajenga hisia za kuwajibika kwa kila mmoja wao. Aidha watakuwa kama jozi moja katika ushirikiano wao badala ya kuwa watu wawili tofauti.

Hitimisho:

Ndoa yaweza kuwa chanzo kikuu cha furaha katika maisha haya na pia, kwa rehema za MwenyeziMungu, inaweza kukuwezesheni kupata Pepo ya Allah Akhera.

Lakini ndoa hiyo hiyo pia inaweza kukuleteeni huzuni katika maisha ya duniani na Akhera. Maisha ya ndoa ni kama ujiti wa ua la waridi ambao huhitaji uangalifu wa hali ya juu. Yashikwe polepole na kwa utulivu ili yastawi na kuchanua.

Ili kufikia shabaha hiyo, waume kwa wake twahitajika kufanya juhudi ya kujielimisha na kudumisha hali ya kujitambua na kujituma. Tuishi kwa kufuata kigezo cha Mtume sallallahu alayhi wa sallam.

1 comment:

  1. Kuna wanawake ambao bado wanaishi kwa miiko ya karne moja nyuma. Hawa wanangoja wanaume zao wawachokoze, wasipofanya hivyo, basi hata mwaka watakaa wakilalamika kwamba hawapati chakula cha usiku. Tukumbuke kwamba hata wanaume nao ni binadamu pia, huhitaji wakati mwingine kushtuliwa, kwani wakishtua wao tu kila siku, kuna wakati hukinai ili ndoa idumu shurti kila mwenye hamu amuanze mwenzie

    Regards

    Lizzy

    ReplyDelete