Monday, August 31, 2009

HOLLYWOOD HAIR THEN AND NOW

    1940: VERONICA LAKE
TODAY: JANUARY JONES
   1950: AUDREY HEPBURN
 TODAY: NATALIE PORTMAN
 1950: LIZ TAYLOR
TODAY:DITA VON TEESE
1970:DIANA ROSS
TODAY: DREW BARRYMORE

RED CARPET

ANJELINA JOLIE
ASHLEE SIMPSON
EVA MENDES
RENEE ZELLWEGER
MICHELL PFEIFFER










      MEGAN FOX

HOTTEST HAIR STYLES

        

MAKOSA YANAYOFANYWA NA WENYE KUFUNGA KATIKA MWEZI WA RAMADHAAN

Yafuatayo ni makosa ambayo yameonekana yakitendeka katika mwezi wa Ramadhaan ima wanapokuwa Waislamu katika Swawm au baada ya kufuturu na katika Swalah za Qiyaamul-Layl. Hivyo inapasa tuyazingatie na kujiepusha nayo ili tubakie katika usalama wa Swawm zetu, Swalah zetu na mengine yote yanayohusu mwezi huu mtukufu:
1. KUTIA NIA KWA KUTAMKA:
 Baadhi wanaamini kuwa nia usipoitamka basi haijawa nia. Na pia huwafunza watoto kutamka maneno ya kutia nia, au kuwaamrisha wasikose kwenda kunuizwa msikitini na mashekhe. Itambulike kuwa nia mahali pake ni moyoni na kutamka ni uzushi.
2.KUFUNGA BILA YA KUSWALI: 
Kufunga bila kuswali: Baadhi ya watu wanafunga bila ya kuswali au kutimiza Swalah ipasavyo. Watu kama hawa Swawm zao hazifai kwani Swalah ni nguzo ya Dini ya Kiislamu.
3.KUDHANI KWAMBA SWALAH YA TAARAWIHY INAANZAWA SIKU YA KWANZA YA RAMADHANI:
Hali inaanza usiku ule unaoandama mwezi. Sunnah ni Waislamu waanze kuswali usiku huo na sio baada ya kufunga siku ya kwanza.
4. KUCHELEWA KUFUTURU/KUFUTARI:
 Baadhi ya watu husubiri hadi adhana imalizike na wengine husubiri hadi kiza kiingie na hali tumehimizwa tukimbilie kufuturu. Matokeo yake ni kukiuka Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia huenda kufanya hivyo wakachelewa Swalah ya Magharibi. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
لا تزال أمتي بخير ما عجَّلوا الإفطار - رواه الإمام أحمد .
((Ummah wangu utabakia katika kheri watakapokimbilia kufuturu)) [Imaam Ahmad]
5. KUOMBA DU'AA ZISIZO SAHIHI WAKATI WA KUFUTURU:
Wengi wameizoea du’aa hii na kuisoma wakati wa kuanza kufuturu, ingawa ni du’aa yenye mapokezi dhaifu yasiyo sahihi:
اَللَّهُمَّ لَكَ صُمْتُ وَ عَلَ رِزْقِكَ أَفْطَرْتُ
Allaahumma Laka Swumtu wa 'alaa Rizqika aftwartu.
6. KUACHA DU'AA SAHIHI:
Du’aa hii ifuatayo ndiyo sahihi iliyohibiti wakati wa kufuturu:
ذَهَـبَ الظَّمَـأُ، وَابْتَلَّـتِ العُـروق، وَثَبَـتَ الأجْـرُ إِنْ شـاءَ اللهُ
Dhahabadh-Dhwama-u Wabtallatil-'Uruuq, Wathabbatal-Ajru Insha-Allaah.
Na hii ni nyingine iliyo sahihi:
اللّهُـمَّ إِنَّـي أَسْـأَلُـكَ بِرَحْمَـتِكَ الّتي وَسِـعَت كُلَّ شيء، أَنْ تَغْـفِرَ لِي
Allaahumma Inniy As-aluka Birahmatikal-latiy Wasi'at Kulla Shay'in An Taghfiraliy.
7. KUFUTURU KWA VITU VYA HARAAM KAMA KUVUTA SIGARA N:K.
Wanakosa kutambua kwamba hii fursa kubwa kwa waliozoea kuvuta sigara kuacha moja kwa moja kuanzia mwezi wa Ramadhaan, kwani ikiwa wameweza kufunga siku nzima na kujizuia kuvuta, vipi washindwe kujizuia na usiku?
8. KULA FUTARI KUPITA KIASI:
Utakuta mtu akifuturu huwa anafanya kisasi, anataka ale kulipiza ile njaa ya siku nzima, matokeo yake anashiba kiasi kushindwa hata kwenda kuswali Taarawiyh.
9. KUKITHIRISHA MICHEZO NA UPUUZI:
 Utakuta watu wakati uingiapo mwezi wa Ramadhaan, ndio wanaanza kutoa ile michezo waliyoiweka pembeni mwaka mzima, au kwenda kununua michezo mipya kama karata, carrum (keram), drafti, domino (dhumna) n.k. wakicheza mchana kutwa ili kupitisha muda uende haraka. Na kisha ifikapo usiku badala ya kwenda kuswali Taarawiyh. Wanakesha kwa kuangalia televisheni, filamu na mipira. Na wengine wakiyaambatanisha hayo kwa kula mirungi na kuvuta sigara. Hayo ni mambo ya haramu na yenye kuwapotezea fadhila na baraka za Ramadhaan, wakati ambapo wangeutumia mchana wao kuchuma kwa kusoma Qur-aan sana na kuhudhuria darsa za Dini au kusoma vitabu vya Dini, kusikiliza mawaidha, Qur-aan au kutazama video za mawaidha n.k. Na ifikapo jioni wangeutumia muda wao kusimamisha Swalah za usiku (Taarawiyh), na pia kupumzika ili waweze kuwahi Swalah ya alfajiri. Gumzo lisilokuwa katika mas-ala ya Dini jambo lililochukizwa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama usimulizi ulivyopokelewa kutoka kwa Abdullah bin Mas-uud (Radhiya Allaahu 'anhu)
عن عبدالله بن مسعود ((لا سمر إلا لمصل أو مسافر))  السلسلة الصحيحة المحدث: الألباني
((Hakuna kupiga gumzo la usiku isipokuwa kwa mwenye kuswali au msafiri)) [As-Silsilat Asw-Swahiyha – Al-Muhaddith Al-Albaaniy]
وعن أبي برزة " أن رسول الله صلى الله عليه وسلم كان يكره النوم قبل
العشاء والحديث بعدها" رواه البخاري ، ومسلم
Na kutoka kwa Abu Barzah kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akichukia kulala kabla ya 'Ishaa na gumzo baada yake) [Al-Bukhaariy na Muslim]
10.KUSENGENYA.KUDANGANYA,KUPIGA POROJO NA KUKAA MABARAZANI KUPOTEZA WAKATI:
 Wanajisahau wengi wetu kwa kupiga soga zisizo na maana na pia kusema wenzao, kutukana, kulaani na kuongea mambo ya uongo n.k. Pia wengi wetu wakifunga huwa na hasira sana. Huko kunapelekea mtu kupoteza ujira wa funga yake na pia hata kuibatilisha (kwa maoni ya Maulamaa wengine), Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: ((Ambaye hatoacha maneno ya uongo na matendo yake, basi ajue kwamba Mwenyeezi Mungu hana haja ya yeye kuacha chakula chake na kinywaji chake)) [ameisimulia Imaam al-Bukhaariy]
11. KUWACHUKUA WATOTO WADOGO MISIKITINI AMBAO WANAFANYA FUJO NA KUSABABISHA KUSHAWISHI MAIMAAM NA MAAMUUMIYN WASHINDWE KUPATA KHUSHUU(UNYENYEKEVU) KATIKA SWALLAH.
 Mwanamke mwenye kuswali nyumbani kwa nia ya kuzuia watoto wake wasilete madhara haya atapata thawabu zaidi kuliko kwenda msikitini na kuleta madhara hayo. Kuwazoesha watoto msikiti ni jambo zuri kabisa, lakini panapoonekana kuna matatizo kama hayo, basi ni bora kuwaepusha ili wasiharibu Swalah za wengi.
12.KUTOKUKAMISHA SWALLAH YA TAARAWIHY:
 Kutokukamalisha Swalah ya Taarawiyh na Imaam ili kupata fadhila za Qiyaamul-Layl kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
(( مَنْ قَامَ مَعَ الإِمَامِ حَتَّى يَنْصَرِفَ كَتَبَ اللَّهُ لَهُ قِيَامَ لَيْلَةٍ))
رواه الترمذي وصححه الألباني في صحيح الترمذي
((Atakayesimama (kuswali) na Imaam hadi amalize ataandikiwa (fadhila za) Qiyaamul-Layl)) [Imesimuliwa na at-Tirmidhiy na kaipa daraja ya Swahiyh al-Albaaniy katika Swahiyh at-Tirmidhiy]
13.KUSHIKA MUS-HAF NA KUMFUATILIZA IMAAM ANAPOSWALISHA:
 Kufanya hivyo, kunamkosesha mtu kuipata Sunnah ya kufunga mikono yake na pia kupoteza fadhila za kuisikiliza Qur-aan kutoka kwa Imaam ambayo tumeamrishwa kuisikiliza inaposomwa, Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((وَإِذَا قُرِىءَ الْقُرْآنُ فَاسْتَمِعُواْ لَهُ وَأَنصِتُواْ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ))
((Na isomwapo Qur-aan isikilizeni na nyamazeni ili mpate kurehemewa)) [Al-A'araaf:204]
14. KUSOMA TASBIY FULANI KILA BAADA YA RAKAA NNE YA MAPUMZIKO:
 Hakuna dalili ya kufanya hivyo. Lililothibiti ni kusoma tasbiyh mwisho kabisa unapomaliza Swalah ya Witr kwa kusema mara tatu:
سُـبْحانَ المَلِكِ القُدّوس
Subhaanal-Malikul-Qudduus
(Kisha kwa sauti ya juu unavuta)
ربِّ الملائكةِ والرّوح
Rabbul-Malaaikati War-Ruuh
15. KUHARAKISHA KULA DAKU:
 Utakuta baadhi ya watu wanawahisha Daku na kuila saa sita za usiku au hata baada tu ya Taarawiyh, ima kwa kutaka walale moja kwa moja hadi alfajiri au kwa sababu ya uvivu wa kuamka kwa ajili ya Daku. Kufanya hivyo ni makosa kwa sababu kunakwenda kinyume na mafunzo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na pia kunapelekea kuikosa ile baraka ya Daku. Na Daku si lazima kula mlo mzito, japo tende au maji yatosha. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
((عجلوا الإفطار ، وأخروا السحور)) صحيح الجامعصححه الآلباني
((Harakisheni kufuturu na chelewesheni daku)) [Swahiyh al-Jaami' na kaipa daraja ya Swahiyh Shaykh Al-Albaaniy]
16. KUDHANI MWISHO WA KULA DAKU NI DAKIKA KUMI KABLA YA ADHANA YA ALFAJIRI
 hivyo mtu akichelewa kula daku na ikawa karibu na dakika chache tu kabla ya Alfajiri hujinyima daku kwa khofu kuwa Swawm yake itabatilika. Wengine wameweka mipaka ya dakika kumi, hivyo si sawa. Mtu anaweza kula daku hadi karibu na Alfajiri hata kunapoadhiniwa. Na pindi Muadhini akiadhini ndipo unapoanza kufunga na Swawm yako inasihi. Na hata Muadhini akiadhini na kama una tonge au fundo la maji mdomoni usiliteme, kamilisha kulimeza kisha ndio uanze kufunga. Haya yamethibiti katika Sunnah kama inavyoonyesha Hadiyth ifuatayo:
Kutoka kwa Sufyaan bin ‘Uyaynah kutoka Az-Zuhriy, naye kutoka kwa Saalim naye kutoka kwa baba yake, kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: ((Hakika Bilaal anaadhini usiku (adhana ya mwanzo), basi kuleni na mnywe hadi aadhini Ibn Ummi Maktuum)) [At-Tirmidhy)
17.KUDHANI KWAMBA MTU ANAPOAMKA NA JANABA HUWA SWAWM YAKE HAIFAI:
 Dhana hiyo si sahihi, bali sahihi ni kuwa mtu anaweza kujitwaharisha hata baada ya kuingia Alfajiri mradi tu aiwahi Swalah ya alfajiri isije kumpita. Na Swawm yake ni sahihi.
18.KUFUNGA UKIWA SAFARINI:
 Walioko safarini kujikalifisha na kujitia katika mashaka ya kufunga na kuacha kuchukua rukhsa iliyotolewa kufuturu; sio jambo jema kufanya hivyo kama ilivyo dalili ya Hadiyth:
عن جابر بن عبدالله أن رسول الله صلى الله عليه وسلم رأى رجلا يظلل
عليه والزحام عليه فقال : ((لَيْسَ مِنَ الْبِرِّ الصِّيَامُ فِي السَّفرَ)) صحيح أبي داود
Kutoka kwa Jaabir bin 'Abdillaah ambaye amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona mtu akiwa amewekwa chini ya kivuli hali yake taabani baada ya kudhoofika kutokana na Swawm akamwambia: ((Sio katika wema (ucha Mungu) kufunga katika safari)) [Swahiyh Abiy Daawuud]
19. KUTOKUJUA HUKMU ZA SWAWM:
 Baadhi ya watu hawajui Hukmu sahihi za funga kisha huwa hawaulizi, ima kwa kuona hayaa au wakidhani wanajua. Ni vizuri mtu aulize lile asilo na hakika nalo kwa wale wenye elimu, ile asije akakosa fadhila na kheri hizi zipatikanazo kwa nadra mno. Na hali ya kutokujua Fiqh ya Swawm, kama kujua mambo yenye kufunguza na yale yasiyofunguza, kunaweza kumpelekea mtu kushinda na njaa bure huku Swawm yake ishabatilika, au kumfanya mtu afungue na hali Swawm yake bado ni sahihi. Mfano wa mambo yasiyobatilisha Swawm ni; kudungwa sindano, kung'oa jino, kujipulizia dawa ya pumu, wanawake kufanyiwa ukaguzi sehemu zao za siri na daktari (gynaecology checkup) - mtu ahakikishe anampata daktari wa kike na akiwa Muislam ndio bora zaidi, na akikosa kabisa hapo ni dharura tena na halaumiwi - na hili si katika Ramadhaan tu, bali ni wakati wowote mwanamke anapokwenda Hospitali awe anafanya jitihada na kuuliza apatiwe daktari wa kike.
20. KUMJUA ALLAAH KATIKA RAMADHAAN PEKEE:
 Baadhi ya watu humkumbuka Allaah katika mwezi huu tu, utakuta wanafunga na kuswali katika Ramadhaan kisha baada ya Ramadhaan kila kitu kinasimama kana kwamba Allaah Hayupo tena! Ni vyema watu wajue kuwa Allaah ni wa miezi yote na si mwezi wa Ramadhaan pekee.
21. KUTAMANI RAMADHAAN IISHE:
Baadhi ya watu wanahesabu masiku na wakiwa wanaomba Ramadhaan imalizike upesi ili warejee katika hali yao ya kawaida ambayo wanaiamini kuwa ina uhuru wa kufanya wanayoyataka. Lau angelijua mja fadhila na kheri zilizo katika mwezi huu, hakika angetamani usiishe.
Katika mwezi ambapo tendo dogo lakuingizia ujira zaidi ya maradufu.
Katika mwezi huu kuna usiku ambao ni bora kuliko miezi elfu.
Katika mwezi huu vishawishi na balaa za Shetani vimewekwa mbali.
Katika mwezi huu Malaika wametapakaa kukusanya amali zako za kheri hata za udogo wa sisimizi
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala Atuongezee elimu ya Dini Yake Tukufu ili tuzidi kutoka katika kiza na kuingia katika mwanga utuongoze katika Swiraatwul-Mustaqiym.

Wednesday, August 26, 2009

NAMNA YA KUTENGENEZA NDOA YENYE FURAHA NA MAFANIKIO

Mara zote vijana na wale wote wanaoowa ama kuolewa huwa na shauku kuu ya kutaraji na kuwa na matumaini kuwa ndoa yao itawaletea maisha yenye furaha.Miezi mitatu mpaka sita baadae wanandoa hawa hubaini kuwa ndoa si jambo jepesi,kumbe ndoa ni jambo linalohitaji subira ya hali ya juu.Vifuatavyo ni vidokezo muhimu vitakavyosaidia mume na mke kujenga mahusiano mazuri na yenye furaha.
1. INGIA KATIKA MAHUSIANO YA NDOA UKIWA NA NIA THABITI,NA KILA MARA IFANYE MPYA NIA YAKO.
Mnapaswa kuyaingia maisha ya ndoa mkiwa na nia safi ya kutafuta radhi za Allah (SW) pamoja na rehma na baraka zake kwa kukusudia kwamba ndoa ni kitu cha kudumu,kufanya hivyo ndoa yenu hugeuka kuwa ibada kitu ambacho kitakuwa kikiwapatia thawabu,nia thabiti ni jambo la msingi litakalowahakikishia amani,umadhubuti wa penzi pamoja na furaha katika muda wote wa maisha yenu ya ndoa.Na kwakuwa tendo hili ni ibada kila mara ifanyeni mpya nia yenu ili kuhakikisha ya kuwa hamtoki nje ya mstari na kukosa faida zitokanazo na uhusiano aupendao Allah (SW)
2. KUMBUKA PIA MKE WAKO NI NDUGUYO KATIKA UISLAMU.
Mara nyingi waislamu wamekuwa wakiwajali zaidi watu wa nje ya familia yao, kwa wema na uaminifu lakini huwa na tabia tofauti kabisa anapokuwa na mwenzi wakehili si jambo zuri kwani hupelekea kuchokana haraka,Waislamu wanapaswa kuelewa kuwa mpenzi wako katika uislamu ni nduguyo,unapaswa kumtimizia kwa kukamiliha wajibu wako.Jitahidi kuzielewa ipasavyo haki za udugu wa kiislamu na kuzifata kimatendo.
3. HIMIZA YALIO BORA KWA MPENZI WAKO.
Kwa kuwa hakuna mwanadamu aliyetunukiwa kila aina ya ubora autakao,basi hamasa iwekwe kwa ule ubora alio nao Asali wako wa moyo,Jitahidi kumtia moyo,kumsifia na kuonesha kuridhishwa na ubora alio nao kila mara,kufanya hivi kutaimarisha ubora wake na kumpa fursa ya kuendeleza vipaji vyengine vya ubora alio nao.Jitahidi kutoyatilia maanani mapungufu madogo madogo aliyo nayo mpenzi wako,yasije kumnyima furaha.''KAMA ALIVYOSEMA MTUME (SAW) KUWA:''MWANAMME MWENYE KUAMINI ASIMDHURU MWANAMKE MWENYE KUAMINI,KWANI ANAWEZA KUCHUKIZWA NA TABIA MOJA LAKINI AKAMPENDA NA KUMRIDHIA KWA TABIA NYENGINE.''(Muslim)
4. KUWA RAFIKI WA KARIBU WA MPENZI WAKO.
Tafakari vipi rafiki wa karibu anapaswa kuwa(best friend) kisha uwe hivyo kwa mwenzi wako,hii inajumuisha kushirikiana katika anavyovipenda,kuujua uzoefu wake,ndoto zake za kimaisha,matatizo yake na hata kukata tamaa kwake.Na hili linawezekana tu pale unapojua mahitaji ya mpenzi wako (anapenda nini hapendi nini) kisha umsaidie kadiri itakavyowezekana.kwani rafiki wa karibu ni mtu unaepaswa kumtunzia siri,kumwamini,kumtegemea katika maisha,hivi ndivyo mpenzi wako anavyohitaji katika maisha yenu ya kila siku.
5. USIWEKE MATARAJIO YASIO WEZEKANA KWA MWANDANI WAKO.
Mara nyingi kabla ya ndoa watu wengi huwa na mawazo ya kinjozi,kuhusu mke au mume mtarajiwa wengi hutegemea kumwona awe amekamilika kila nyanja,katika uhalisia ni vigumu kumpata mtu aliye kamilika kwa kila jambo.Vinginevyo mawazo hayo husababisha kero na matatizo yasio na muhimu katika ndoa yako.Yafaa tuzingatie Allah( sw) amemjaalia mwanadamu kuwa ni mwenye mapungufu mengi hivyo tutegemee kasoro nyingi,kwa kuzingatia hili la mapungufu ya kibinadamu na kujitahidi kwako kurekebisha mapungufu hayo ya mwenzio,basi uatashangazwa na kuona ndoa yenu itakavyokuwa na maridhiano.
6.TUMIENI MUDA WA THAMANI PAMOJA.
Mnapaswa kutafuta muda wa ziada katika ratiba zenu ngumu za kimaisha ,kuimarisha penzi lenu kwa kuwa pamoja,na muda wa thamani unaokusudiwa hapa ni kama vile kufanya safari fupifupi pamoja ,au hata kufanya shughuli itakayoruhusu uwili wenu nje ya maisha ya nyumba yenu na mengine mengi mfano wa hayo.
7. ONESHA HISIA ZAKO MARA ZOTE.
Njia ya mawasiliano yenu yapaswa kuwa wazi na tayari kupokea hisia za mwenzi wako kila zinapoibuka,hii nitiba mujarab ya nafsi,Lakini kuna hatari kubwa kunyamazia hisia za mwenzi wako hasa za kimapenzi.Jitahidini kukidhiana haja.
8.KIRI MAKOSA NA JENGA TABIA YA KUOMBA MSAMAHA.
Kama tufanyavyo katika kumuomba Allah (sw) msamaha kila mara tukoseapo,hivyo ndivyo tunapaswa kufanya kwa wapenzi wetu,kwani mtu mara na mwenye nguvu ni yule ambae yuko tayari kukiri pale anapokosea,na kisha kuomba msamaha.Baada ya hapo ongeza juhudi kuboresha yale yote yanayoongeza mapenzi,mwanandoa asiye tayari kufanya hivi ategemee maendeleo duni yakimahaba katika ndoa yao.
9.USIPENDE KUIBUA MAKOSA YA WAKATI ULIO PITA.
Uislamu unakataza mtu kujikita na kusimamia mambo yalio kwisha pita.Mtu anapaswa ayakumbuke makosa yaliyopita ili yasije yakarejewa tena,lakini hili lisiwe linafanywa kupita kiasi,bila shaka sisi kama binadamu hatuna haki yakuwahukumu bianadamu wenzetu.twaweza kuwashauri tu tena kwa kuzingatia maadili.
10.BAADHI YA WAKATI MSTAAJABISHE MKE WAKO.
Kuna namna nyingi za kumstaajabisha mpenzi wako,kama kumlete zawadi ndogondogo au hata katika muda ambao hakuutegemea,au kumuandalia mlo maalum au kumvalia mavazi ya kupendeza au kujipendezesha,kwa naman nyengine yoyote aipendayo mahabubu wako,hii ni ka wanawake na wanaume. Lengo kuu ni kuyatia ladha mapenzi na uhusiano wenu wa kindoa kwa kuepusha kwa kupesha ratiba zenye kuchosha.
11.KUWA NI MWENYE MZAHA NA UTANI BAADHI YA NYAKATI.
Uchangamfu,ucheshi,na utani usiopindukia mipaka ya uislamu kwani ni miongoni mwa mambo yanayoongeza ladha ya mapenzi katika ndoa,utani huzuia mabishano na hufungua nuru ya mapenzi katika familia,Kwa kuwa maisha ni mkondo wenye changamoto nyingi na mitihani,kuyaendea vyema maisha hayo humuia rahisi yule mwenye moyo mkunjufu na uliojaa maskhara ya kimapenzi.Hata kama upatikanaji riziki yenu ni mdogo basi utamuona mwandani wako hachoki kuwa nawe popote utapokwenda.

MAFANIKIO KATIKA NDOA

Badala ya watu kuangalia dosari katika ndoa za wengine, kwanini wasitazame mafanikio katika ndoa nyingine. Kuna mengi ya kujifunza badala ya mengi ya kukosoa.

Wengi hupenda kutazama ndoa zilizofeli, wakijaribu kudadisi kwa nini ndoa hizo zimeshindwa na lengo lao sio kutoa msaada bali lengo ni kufurahisha genge. Lakini jambo la ajabu watu hao huzifumbia macho ndoa zilizofanikiwa.

Katika makala haya, tutajaribu kutoa ushauri uliotokana na utafiti ili watu watazame zaidi ndoa zilizofaulu na kuyatambua mambo ya msingi yanayojenga na kudumisha maisha mema ya ndoa.

Sisi, kwa kuyatazama mambo haya ya maana, tumebaini virutubisho muhimu vya maisha ya ndoa ambavyo vinaweza kumpatia kila mwanandoa furaha inayotafutwa mno katika maisha hayo. Hapa kuna mambo manane:

1. Dhati ya moyo na Upendo wa dhati (Eternal Commitment and caring)

Ndoa zinazojengwa kwa msingi wa dhati ya moyo (commitment) huwa katika mazingira ya usalama ambayo huwapa wanandoa wasaa wa kujistawisha na kufanikiwa kwa kiwango kinachozidi uwezo walionao.

Nao upendo wa dhati maana yake ni hisia za kila mmoja kumjali mwingine pengine kuliko hata anavyoijali nafsi yake. Hisia hizi hufuta ubinafsi moyoni na kumfanya kila mmoja aangalie shida na mahitaji ya mwingine kuliko anavyoangalia shida na mahitaji yake binafsi.

Mume na mke waishi katika mawimbi ya hisia kila mmoja ajaribu kumzidi mwingine hisia za kumjali mwenza, hapa maisha ya ndoa yatakuwa ya furaha kwelikweli na ndoa hiyo, InshaAllah, itadumu na kama itavunjika basi ni kwa sababu za msingi za kibinadamu.

Wanandoa katika ndoa za namna hii, mara nyingi, hutenganishwa na kifo. Ndoa hizi huwa na mvuto kwa wengine na huandaa mazingira bora ya kizazi kipya ambacho, kwa vyovyote, kitakuwa na nguvu kubwa ya maadili itakayowavutia wanajamii kwa ujumla.

Lakini ubinafsi wa kila mmoja kujitazama yeye tu bila kumjali mwenza huondosha imani ya kila mmoja kwa mwingine na hujenga mtindo mbaya wa ‘chukua chako, nichukue changu’

Kila mmoja hutanguliza mbele maslahi yake na humtimizia mwingine haja zake pale anapoona kuna maslahi kwake. Wanandoa hufikia mahala pa kuwekeana masharti, bila mmoja kufanya kitu fulani basi mwingine naye hawezi kufanya kitu fulani. Hata unyumba hufanyika kwa masharti.

Kwa hiyo basi, dhati ya moyo na upendo wa dhati ndizo sifa za msingi za ndoa yenye mafanikio. Msukumo ulio nyuma ya sifa hizi ni uadilifu. Uadilifu wa wanandoa ndio unaoimarisha ndoa na kuipa nguvu ya kudumu.

Ni jambo la kuzingatia mno kuwa ndoa ni mkataba lakini mkataba huu hauna uhai wa kujitegemea, uhai wa mkataba huu si wa cheti cha ndoa wala si wa sherehe za harusi bali umo katika nyoyo za wale wanaoufunga.

Ndoa, katika Uislamu, ni mkataba baina ya wanandoa. Huu ni mkataba ambapo kila upande lazima uwajibike na majukumu yake. Tija ya mkataba huu wa hiyari hutegemea athari za kupendana na kuhurumiana kwa wanandoa.

Wanandoa jengeni maisha yenu ya ndoa sio kwa mapenzi yanayoambatana na masharti bali kwa utamaduni wa hisani. Toa kwa ajili ya Allah kwanza halafu toa kumpa mwenza bila kutarajia kurejeshewa malipo yoyote kutoka kwake.

Kila mwanandoa mwenye moyo wa dhati ashirikiane na mwenza kutekeleza majukumu ya msingi na kufanya kazi za kila siku. Kila mmoja ajitahidi kuonesha ushirikiano wa asilimia 100.

Kigezo chetu bora ni maisha ndoa ya Mtume sallallahu alayhi wa sallam na Bi Khadija. Bi Khadija alimsaidia Mtume kwa mali yake na akamsaidia nyumbani.

2. Mawasiliano bora (Effective Communication Skills)

Mawasiliano ni muhimu zaidi kuliko maelewano. Wanandoa wanaweza kutofautiana mara nyingi lakini bado wakadumisha ndoa yao iwapo watawasilishiana hisia na fikra zao kwa njia bora.

Miaka ishirini na mitano ya utafiti inatubainishia kuwa mafanikio katika ndoa hayahusiani sana na aina ya tofauti baina ya wanandoa. “Ukitaka kuwa na ndoa yenye furaha, basi ni vema ujuwe zaidi njia ya kuyadhibiti mambo yanayoleta tofauti hizo kuliko hata kuzijua tofauti zenyewe”, hivi ndivyo wasemavyo Madaktari hawa, Dkt.Markman, Stanley na Blumbarg katika kitabu chao “Fighting for Your Marriage”

Kuweka wazi njia za mawasiliano baina ya wanandoa ili kubadilishana hisia zao nzuri na mbaya ni jambo muhimu mno. Wasilisha mawazo yako vizuri iwe kuhusu jambo jema au tatizo, eleza kwa lugha nzuri yale unayoyakubali na tumia lugha nzuri zaidi na ya hekima kueleza yale unayoyakataa.

Pale inapojitokeza hali ya kutoelewana, fanyeni mazungumzo ya wazi kudhibiti hali ya mambo mkitumia stratejia ya kulishinda tatizo, ‘win-win strategy’

Katika programu yake Mashuhuri ya Mafunzo iitwayo, “seven Habits of Highly effective People”, “Tabia Saba za Watu wenye busara ya hali ya juu”, Bw. Steven Covoy anasema, “Win-Win”is a paradigm of human interaction that comes from integrity, maturity and abandance mentality.”Busara ni mabadiliko katika maisha ya mwanadamu ambayo huja kutokana na uadilifu, upevu na wingi fikra.”

Kwa mawasiliano bora unaweza kukifikia kiwango cha unyumba (intimacy) unachokitaka. Mahusiano na mashirikiano bora katika nyumba huwezekana iwapo mume na mke watakuwa wazi kwa kila mmoja wao. Pale kila mmoja wao anapomuamini mwenziwe na anapoaminiwa na mwenza, wote wawili huweza kuwasilishiana fikra na hisia zao bila kitete (reservation).

3. Amani ya Hisia (Emotional Safety)
“Kuonesha amani ya hisia ni jambo la msingi katika kujenga mahusiano ya dhati ya ndoa yenye mapenzi ambayo wewe unaitaka.” Hivi ndivyo wanavyosema Madaktari, Markman, Stanley na Blumberg.

Hapa wana maana ya mume na mke kuishi kwa heshima, huruma na mapenzi. Pale wanandoa wanapokumbana na tatizo au hali fulani ngumu iwe ya nje au ya ndani, wafanye kila jitihada kujizuia na ghadhabu na kinyongo.

Katika nyakati hizi ngumu, wajitahidi kufichiana siri na kusitiriana. MwenyeziMungu anasema wao (wanawake) ni nguo kwenu na nyinyi ni nguo kwao”. (2:187).

Wanandoa Waislamu wasaidiane hasa hasa katika nyakati ngumu. Pale watu wengine wanapomtelekeza, basi mtu hujirudisha kwa mwandani wake ili apate kumfariji na kumpa nguvu ya kukabiliana na hali ngumu aliyonayo na kuendelea na safari yao ya maisha.

Mama wa Waumini yaani wakeze Mtume sallallahu alayhi wa sallam walikuwa karibu na Mtume katika matatizo na mapambano aliyokabiliana nayo.



4. Kudumu na matarajio halisi (Developing Realistic Expectation)

Achana na njozi (ideal image) ya kuwa na mume ambaye hawezi kupatikana katika dunia hii. Ndugu yetu mmoja katika Uislamu alielezea uzoefu na uchunghuzi wake katika miaka miwili ya ndoa yake akisema; “The fastest path to destroying one’s marriage is false hopes and ideals that we make for ourselves. For instance, we may think that another couple’s relationship is our inspiration and a model to copy. This may bring positive results in some instances and can lead to crisis in others”

Yaani “njia ya haraka zaidi ya kuvunja ndoa ya mtu ni imani na mawazo potofu tunayoyajenga sisi wenyewe (wanawake). Mathalani, tunaweza kudhani kuwa ndoa ya watu wengine ndiyo ya kutuongoza na ndio kigezo cha kuiga.. Hii yaweza kuleta tija katika ndoa fulani na kusababisha matatizo katika ndoa nyingine.”

5. Kuyaangazia mambo mema (Shining a Light on What is Right)

Tabia njema kwa mwenza ni moja ya zawadi ambazo mume na mke wanaweza kuiletea ndoa yao. Kwa kuridhiana, mume na mke humfanya kila mmoja wao kuwa mpenzi mkubwa wa mwingine.

“Hapa kuna msemo mmoja unaowahusu waume na wake, “kama unataka kumbadili umpendae, basi mpende. Kama mapenzi yako ni ya kweli, basi mumeo au mkeo atayahisi na yeye atashawishika moyoni kupenda, kujali na kuwa msaidizi.

6. Kuhisi na kuzingatia hisia na mahitaji ya mwenza (Sensitivity and Consideration to the spouse’s feelings and needs)

Igeuze kanuni hii, “Mtendee mwandani wako kama wewe unavyotaka kutendewa.” Badala yake fuata kanuni ambayo ni bora zaidi, “mtendee mwandani kama anavyotaka kutendewa.”

Jambo hili ni rahisi kulisema lakini gumu kulitenda. Ni jambo linalohitaji ufahamu sahihi na maridhiano ya kweli ya wanandoa. Jaribu kung’amua mambo yanayomfurahisha mwenza kwa kuyasoma maongezi yake mwenyewe.

Tia tone la maji katika ndoo ya mwandani wako ili kutia nyongeza katika benki ya hisia ya mwenza. Katika kitabu chao “How Full Is Your Bucket? Positive Strategies for Work and Life, Tom Rath na Donald Clifton waliutazama utafiti wa miaka hamsini wa Gallup pamoja na mamilioni ya mahojiano kuweza kujenga hoja kuwa uhusiano huu ‘wa nipe-nikupe’ give-and-take hujenga ndoa imara, huzidisha furaha na tija kwa mfanyakazi na hujenga ulimwengu wenye furaha zaidi.

Nadharia yao inasema hivi: “kila mmoja wetu ana ndoo yake iliyofichikana ambayo huwa tupu au hujaa katika maisha ya kila siku, hii hutegemea watu wengine wanavyotusemesha au kutufanyia jambo.

Ndoo yetu inapokuwa imejaa, tunakuwa na furaha, na ndoo yetu inapokuwa tupu, tunasononeka. Kila mmoja wetu pia ana kata lisiloonekana. Tunapotumia kata hiyo kujaza ndoo za wengine-kwa kusema au kufanya mambo yanayowapunguzia hisia njema- basi tunajipunguzia hisia hata sisi wenyewe.”

Wanandoa wanaofaulu kufahamu kila mmoja wao anahitaji nini ndio wenye uwezekano zaidi wa kuijiongezea kiwango cha hisia katika benki ya hisia. Katika mchakato huu tunatakiwa kujifahamu kabla ya kufahamika, kujielewa kabla ya kueleweka, kujitambua kabla ya kutambuliwa.

Ili kuweza kufanya hilo, jaribu kusikiliza kwa hisia. Epukeni kukaripiana, kupelelezana, kudhaniana na kukisiana.

7. Urafiki (Companionship)

Urafiki muhimu na wa kudumu muda mrefu ni ule wa wanandoa. Takribani yale yote yanayohusiana na uhusiano wa urafiki yamo katika uhusiano wa ndoa isipokuwa zipo tofauti.

MwenyeziMungu kawapangia mume na mke kuwa marafiki wa ndani. Mume na mke wanapokuwa marafiki, huweza kusaidiana kuikabili changamoto ya Uislamu ya kuishi kwa kufuata misingi na maadili yake ili kupata furaha katika dunia hii na Akhera.

MwenyeziMungu Anasema, “Na wanaoamini wanaume na wanaoamini wanawake ni marafiki wao kwa wao. Huyaamrisha yaliyo mema na kukataza yaliyo mabaya, na husimamisha Sala na hutoa Zaka na humtii MwenyeziMungu na Mtume Wake. Hao ndio ambao MwenyeziMungu atawarehemu. Hakika MwenyeziMungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima. (9:71).

Ili kufaulu kufikia lengo hili tukufu, tuache matamanio ya nafsi zetu na majivuno, na badala yake tuitazame dini yetu bila kujali nani anayeizungumzia, mwanaume au mwanamke, mzee au kijana mwanazuoni au mtu wa kawaida.

Tuipime hoja yake na kuitafutia uthibitisho wa Qur’an na Hadith Sahihi. Aidha inahitaji tujiepushe na athari za mazoea, maslahi binafsi na ubinafsi.

8. Kupanga ratiba (Making a schedule)

Kupanga ratiba kunatoa nafasi ya kuendesha maisha yenu kwa mpangilio bora. Hii hasa huwa muhimu zaidi iwapo mume na mke wanasoma au kufanya kazi.

Katika hali hii ratiba husaidia kutenga muda kwa kila mmoja katika siku za kazi na masomo. Ratiba inaweza kujumuisha mambo haya.

-Kusali pamoja angalau kipindi kimoja cha Sala
-Kuhudhuria pamoja darasa-duara mara moja kwa wiki.
-Kutenga siku moja ambapo kusiwe na kazi wala masomo, na badala yake kushughulika na yale yanayompendeza kila mmoja.
-Kutenga siku moja ambapo mume na mke kwa pamoja wafanye kazi ya usafi wa nyumba.
-Kutenga siku na muda wa kutembelea ndugu, jamaa, wagonjwa.
-Kutenga muda wa kujadili bajeti na kutatua matatizo.

Kwa kujipangia ratiba hii, wanandoa watajenga hisia za kuwajibika kwa kila mmoja wao. Aidha watakuwa kama jozi moja katika ushirikiano wao badala ya kuwa watu wawili tofauti.

Hitimisho:

Ndoa yaweza kuwa chanzo kikuu cha furaha katika maisha haya na pia, kwa rehema za MwenyeziMungu, inaweza kukuwezesheni kupata Pepo ya Allah Akhera.

Lakini ndoa hiyo hiyo pia inaweza kukuleteeni huzuni katika maisha ya duniani na Akhera. Maisha ya ndoa ni kama ujiti wa ua la waridi ambao huhitaji uangalifu wa hali ya juu. Yashikwe polepole na kwa utulivu ili yastawi na kuchanua.

Ili kufikia shabaha hiyo, waume kwa wake twahitajika kufanya juhudi ya kujielimisha na kudumisha hali ya kujitambua na kujituma. Tuishi kwa kufuata kigezo cha Mtume sallallahu alayhi wa sallam.